Kihongosi Azindua Msimu mpya wa Mazoezi Arusha, atoa wito Kujenga Taifa lenye Afya na Umoja - PAMWASH BLOG

Jamii Yetu , Maisha Yetu

Saturday, 19 July 2025

Kihongosi Azindua Msimu mpya wa Mazoezi Arusha, atoa wito Kujenga Taifa lenye Afya na Umoja


Na Frida Maganga,Arusha 

Wakazi wa Jiji la Arusha wamejitokeza kwa wingi leo Julai 19, 2025, kushiriki katika uzinduzi wa msimu wa pili wa Arusha Jogging Sports uliofanyika kwa kishindo chini ya uongozi wa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Kenan Kihongosi. Zoezi hilo la mazoezi ya kukimbia kwa umbali wa kilomita 10 limevuta washiriki wa rika mbalimbali, likilenga kuimarisha afya ya mwili sambamba na kujenga mshikamano wa kijamii.

Katika uzinduzi huo ulioandaliwa na Arusha Jogging Club, Mkuu wa Mkoa aliongoza maandamano ya mazoezi kuanzia ofisi yake hadi maeneo ya katikati ya jiji na Mianzini kisha kurudi, huku wakisindikizwa na askari wa usalama barabarani. Tukio hilo limekuwa jukwaa muhimu la kuhimiza amani, mshikamano, na uzalendo miongoni mwa wakazi wa Arusha.

Akizungumza baada ya mazoezi hayo, Mhe. Kihongosi aliwataka wakazi wa Arusha kuishi kwa upendo, mshikamano na kudumisha amani pasipo kubaguana kwa misingi ya dini, kabila au itikadi za kisiasa. 

Amesema baadhi ya watu wenye nia mbaya wamekuwa wakitafuta njia ya kuwagawa wananchi kwa faida zao binafsi, jambo ambalo halipaswi kuvumiliwa.

Katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu mwezi Oktoba,Kihongosi aliwahimiza wakazi wa Arusha kujitokeza kwa wingi kupiga kura, huku akiwataka kutopokea maneno ya kukatishwa tamaa au kushawishiwa kutoshiriki katika zoezi hilo muhimu 

Uzinduzi wa msimu huu wa pili wa Arusha Jogging Sports umepokelewa kwa shangwe kubwa na wakazi wa Arusha, ambapo wengi wameelezea kuwa mazoezi hayo si tu yanachangia afya bora, bali pia ni jukwaa la kukuza mshikamano, uzalendo na maadili ya kijamii. 

Mkuu wa Mkoa pia aliipongeza Arusha Jogging Club kwa juhudi zao katika kuhamasisha mazoezi kwa jamii na kuwataka waendelee kuibua vipaji na kuimarisha afya kwa njia chanya na jumuishi.
WhatsApp%20Image%202025-07-19%20at%2009.09.37
WhatsApp%20Image%202025-07-19%20at%2009.09.38
WhatsApp%20Image%202025-07-19%20at%2009.09.39
WhatsApp%20Image%202025-07-19%20at%2009.09.40
WhatsApp%20Image%202025-07-19%20at%2009.09.41%20(1)
WhatsApp%20Image%202025-07-19%20at%2009.09.41%20(2)
WhatsApp%20Image%202025-07-19%20at%2009.09.41
WhatsApp%20Image%202025-07-19%20at%2009.10.38
WhatsApp%20Image%202025-07-19%20at%2009.10.39

No comments:

Post a Comment

HABARI