Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngoyani ametoa Miezi sita kwa wakazi wa Mpanda Mkoani Katavi kuondoka katika maeneo ya hifadhi za Reli ili kupisha maboresho yanayoendelea kufanywa na Shirika la Reli Tanzania (TRL) kwenye miundombinu yake.
Ametoa agizo hilo wakati akiongea na wafanyakazi wa taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo Mkoani Mpanda na kusema ni wakati sasa kwa wananchi kufuata sheria kwa kutovamia miundombinu hiyo.
“Ninatoa miezi sita kuanzia sasa, itakapofika Mwezi Januari mwakani wananchi wote watakaokuwa ndani ya hifadhi ya reli watabomolewa nyumba zao kwa kuzingatia sheria zinazolinda miundombinu,” alisisitiza Eng. Ngonyani.
Naibu Waziri Eng. Ngonyani ameuagiza uongozi wa Mkoa wa Mpanda kusimamia zoezi la wananchi kuhama na kuhakikisha kila aliyevamia miundombinu hiyo anabomoa nyumba yake kabla ya sheria kufata mkondo wake.
Aidha, Eng. Ngonyani amewatahadharisha wafanyakazi wa Wakala wa barabara nchini (TANROADS) kuzingatia maslahi mapana ya Taifa wakati wa kutafuta zabuni kwa kufanya hivyo watakuwa wanamuunga Mkono Mhe. Rais Dkt. John Magufuli.
Katika hatua nyingine Eng. Ngonyani amekagua barabara ya Kanazi-Kizi-Kibaoni (76.6KM), Sumbawanga-Kanazi (75KM) ambapo ameiagiza TANROADS Mkoa wa Rukwa kuweka mizani katika barabara zinazojengwa ili kudhibiti magari makubwa yanayozidisha uzito na kusababisha uharibifu kwa barabara katika Mkoa huo.
“Ni wakati sasa wanaotoa huduma za usafirishaji wa mizigo kufuata sheria na kubeba mzigo wa uzito unaostahili sababu madereva hao hao wakienda nchi za jirani wanafuata sheria kwa umakini, SUMATRA simamieni utoaji wa leseni kwa magari ya abiria na mizigo kwa kuzingatia uzito wa magari ili kuziweshesha barabara zetu zidumu,” alisisitiza Eng. Ngonyani.
Kwa upande wa Meneja wa TANROADS Mkoa wa Rukwa, Eng. Msuka Mkina amemuhakikishia Naibu Waziri kuwa Wakala utahakikisha Mizani inawekwa sehemu za barabara ili kubaini Magari yanayozidisha uzito na kuyachukulia hatua za kisheria.
Naibu Waziri Eng. Ngonyani yupo katika Ziara ya kukagua Miundombinu ya barabara, Viwanja vya Ndege, Ujenzi wa Nyumba za viongozi, huduma za mawasiliano ya simu na Madaraja katika Mkoa wa Katavi na Rukwa.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani akitoa maelekezo kwa Meneja wa Kampuni ya Simu (TTCL) mkoa wa Rukwa na Katavi Bw. Peter Kuguru wakati alipokagua eneo ambalo Mkongo wa Taifa umeharibika kwa kuliwa na panya Wilayani Nkasi Mkoani Rukwa.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani (Katikati) akiangalia ramani ya Mkongo wa Taifa wakati alipokagua eneo ambalo Mkongo wa Taifa umeharibika kwa kuliwa na panya Wilayani Nkasi Mkoani Rukwa.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani (Kulia) akitoa maelekezo kwa Mkandarasi anayejenga barabara ya Kanazi-Kizi-Kibaoni (76.6KM) Wakati alipokagua ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami.
Meneja wa Kampuni ya Simu (TTCL) mkoa wa Rukwa na Katavi Bw. Bw. Peter Kuguru (aliyenyoosha kidole) akifafanua jambo kwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani wakati alipokagua eneo ambalo Mkongo wa Taifa umeharibika kwa kumegwa na panya Wilayani Nkasi Mkoani Rukwa.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Edwin Ngonyani (Kulia) akipokea maelezo ya kifaa maalumu cha kugundua sehemu ambayo mkongo wa Taifa una tatizo kutoka kwa Bw. Juma Ngimba (Kulia), wakati alipokagua eneo ambalo Mkongo wa Taifa umeharibika kwa kuliwa na panya Wilayani Nkasi Mkoani Rukwa.
Muonekano wa barabara ya Kanazi-Kizi-Kibaoni (76.6KM), ambayo ujenzi wake kwa kiwango cha lami umekamilika.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
No comments:
Post a Comment