(Jumanne, Machi 25, 2025 – Arusha)
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Christian Makonda, leo amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Bw. Masanja Kadogosa, kuhusu mpango wa ujenzi wa reli ya kisasa ya Standard Gauge Railway (SGR) itakayounganisha mikoa ya Kaskazini.
Katika mkutano huo uliofanyika ofisini kwake Jijini Arusha, Bw. Kadogosa alieleza kuwa serikali tayari imeanza taratibu za ujenzi wa reli hiyo, mradi unaotekelezwa chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kama sehemu ya maono ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere. Ujenzi huu unalenga kuboresha miundombinu ya usafirishaji na kukuza uchumi wa Mkoa wa Arusha na kanda nzima ya Kaskazini.
Akizungumza kuhusu manufaa ya mradi huo, Bw. Kadogosa alisema kuwa reli hiyo ya kisasa itakuwa chachu ya maendeleo kwa Arusha, hasa kwa sekta ya uchumi, biashara na madini. Alifafanua kuwa uwepo wa madini ya soda katika mkoa huo ni rasilimali muhimu, huku akibainisha kuwa machimbo ya madini hayo yana uwezo wa kudumu kwa zaidi ya miaka mia moja. Aidha, alieleza kuwa ujio wa bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Tanga utahitaji mfumo madhubuti wa usafirishaji wa mafuta ghafi, na reli hii itakuwa njia mojawapo muhimu ya kusafirisha mafuta hayo hadi masoko ya kimataifa.
Kwa upande wake, Mhe. Makonda alimshukuru Rais Samia kwa uwekezaji mkubwa unaofanyika katika Mkoa wa Arusha, akiahidi kuwa wakazi wa mkoa huo wataendelea kuunga mkono juhudi za maendeleo zinazoletwa na serikali ya awamu ya sita. Pia, alisisitiza kuwa Arusha imejipanga kuweka rekodi kwa idadi kubwa ya kura kwa Rais Samia katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu kama ishara ya shukrani kwa miradi inayotekelezwa, ikiwemo ukuzaji wa uchumi, uimarishaji wa sekta ya utalii na madini, na kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara.
Katika hatua nyingine, Mhe. Makonda alibainisha kuwa Mkoa wa Arusha kwa kushirikiana na Wizara ya Madini umeanza maandalizi ya maonesho ya madini yatakayofanyika kila mwaka, hatua itakayosaidia katika kutangaza na kuendeleza sekta ya madini nchini.
No comments:
Post a Comment