MTANDAO ya Jinsia Tanzania (TGNP) leo imeweka hadharani malengo makuu ya Tamasha la Jinsia la mwaka 2017 linalotarajia kuanza rasmi Septemba 5 hadi 8 ya mwaka 2017 katika viwanja vya TGNP Mabibo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TGNP, Vicensia Shule alisema tamasha la mwaka huu litakuwa na malengo manne na lengo la kwanza ni kutafakari na kusherehekea mafanikio, changamoto zilizopo katika kuendeleza usawa wa kijinsia. Alisema hili ni kuzingatia utekelezaji wa mikataba, maazimio, sera na mikakati mbalimbali ya kimataifa.
Alisema lengo la pili ni kutathmini ushiriki wa wanawake katika michakato ya kufanya maamuzi katika uongozi, hususan uongozi wa kisiasa kwenye Serikali za mitaa. Lengo la tatu ni pamoja na kufuatilia kuhifadhi, kutambua na kusherehekea viongozi wanawake wenye michango ya kuigwa juu ya usawa wa kijinsia na uwezo wa wanawake, hususan mapambano dhidi ya mfumo dume na uliberali mamboleo.
Akifafanua kuhusiana na lengo la tatu, Bi. Vicensia Shule alisema katika lengo hili TGNP itawatambua na kuwapongeza wanawake waliofanya vizuri maeneo mbalimbali akiwemo Makamu wa Rais wa Tanzania, Bi. Samia Suluhu, Spika mstaafu wa Bunge la Tanzania, Anna Makinda, Mbunge wa Bunda Mjini, Estar Bulaya, Mama Getrude Mongela, Dk. Ester Mwaikambo, na Msanii Fatma Baraka (Bi. Kidude) kwa jitihada walizozionesha katika uongozi.
Aidha alisema lengo la nne itakuwa kuhimarisha harakati za ukombozi wa wanawake kimapinduzi kupitia ujenzi wa nguvu za pamoja. “…Tamasha la Jinsia la mwaka huu litaongozwa na mada kuu isemayo ‘Mageuzi ya mifumo kandamizi kwa usawa wa kijinsia na maendeleo endelevu'” alisema Bi. Vicensia Shule.
No comments:
Post a Comment