KIWANDA CHA KUZALISHA HOJA NI WATENDAJI WA HALMASHAURI; DKT NCHIMBI. - JAMII BLOG

Jamii Yetu , Maisha Yetu

Post Top Ad

Responsive Ads Here

Wednesday, 19 July 2017

KIWANDA CHA KUZALISHA HOJA NI WATENDAJI WA HALMASHAURI; DKT NCHIMBI.





Watendaji wa halmashauri za wilaya na manispaa wamekuwa ni kiwanda cha kutengeneza hoja za mkaguzi na Mthibiti Mkuu wa hesabu za Serikali kwa kukosa umakini, uaminifu, uwajibikaji na kutokuzingata sheria, kanuni na maadili ya utumishi wa umma.


Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema ameyasema hayo mapema leo katika baraza maalumu la madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya Ikungi wakati wa kujadili hoja 80 za Mkaguzi na Mthibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka 2015/16 licha ya halmashauri hiyo kupata hati safi.


Dkt Nchimbi amesema wamekuwa ndio wazalishaji wakubwa wa hoja tena hoja zenyewe zikionyesha udhaifu wao wa kutotimiza wajibu wao huku akiwaeleza kuwa hoja hizo zinaonyesha kuwa kuna udhaifu katika utendaji wao.


“Hoja hazitengenezwi na madiwani, ni nyinyi watendaji kwa uvivu, mnashindwa kufuata taratibu hadi mnazalisha hoja, mmekuwa ni kiwanda na kiwanda chenyewe kibaya cha kuzalisha hoja, badilikeni”, amesisitiza Dkt Nchimbi.


Aidha amewataka madiwani kuwa wasimamizi wa miradi na shughuli za serikali pamoja utendaji wa watumishi ili wasiendelee kuzalisha hoja kwakuwa utendaji ukilega lega unawaathiri wananchi ambao ndio wamewaamini ili wawakilishe.


Dkt amewasisitiza kuwa watumishi wengine huja na kuondoka lakini madiwani ndio wazawa hivyo maendeleo yao wanapaswa kuyasimamia kwa nguvu zote wakishirikiana na watumishi pamoja na kuwashauri viongozi wa halmashauri katika kuboresha utendaji.


Amewataka madiwani pia kuwasimamia watumishi wasijiingize kwenye ushabiki wa kisiasa na kupandikiza chuki kwa wananchi bali wao wajikite kwenye kuhudumia wananchi na kuwaachia siasa madiwani na wanasiasa wengine.


Naye Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt Angelina M Lutambi ameishauri halmashauri hiyo kuhakikisha wanafunga hoja hizo ili halmashauri hiyo iendelee kupata hati safi.


Dkt Lutambi amesema watumishi wasijisahau na kufanya kazi kwa mazoea bali wachape kazi kwa bidii, kwa ubunifu na kwa kufuata taratibu ili kutoa huduma nzuri kwa wananchi na kuepuka kuzalisha hoja.Ameongeza kuwa taifa na halmashauri ya Ikungi inazo rasilimali za kutosha, jukumu la watumishi ni kuhakikisha rasilimali hizo zinawanufaisha wananchi wote bila upendeleo au kuzifuja.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Rustika Turuka amesema yeye na watendaji wake wote watahakikisha wanazingatia ushauri na maelekezo yaliyotolewa katika baraza hilo ili hoja zifutwe.


Turuka ameongeza kuwa atahakikisha halmashauri ya Ikungi haipati hoja nyingi na itaendelea kupata hati safi kama ambavyo imekuwa ikipata kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo.


Amesema kuwa atashirikiana na madiwani katika kuhakikisha halmashauri inakusanya mapato yake vizuri na kuongeza vyanzo vingine vya mapato ili waweze kutoa huduma kwa wananchi kwa ajili ya maendeleo ya Ikungi na taifa kwa ujumla.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akizungumza katika baraza maalumu la madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya Ikungi wakati wa kujadili hoja za Mkaguzi na Mthibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali. Kulia kwake ni Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Jumanne Mtaturu na Kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Ally Mwanga.

Watumishi wa halmashauri ya Wilaya ya Ikungi wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi katika baraza maalumu la madiwani la kujadili hoja za Mkaguzi na Mthibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali.



Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Rustika Turuka akizungumza katika baraza maalumu la madiwani la kujadili hoja za Mkaguzi na Mthibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya Ikungi katika baraza maalumu la madiwani la kujadili hoja za Mkaguzi na Mthibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad

Responsive Ads Here