PROF. MBARAWA: FIDIA ZITALIPWA KWA WANAOSTAHILI KISHERIA - JAMII BLOG

Jamii Yetu , Maisha Yetu

Post Top Ad

Responsive Ads Here

Tuesday, 18 July 2017

PROF. MBARAWA: FIDIA ZITALIPWA KWA WANAOSTAHILI KISHERIA







Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kulia), akipokea taarifa kutoka kwa Mkandarasi wa Kampuni ya CHICO (katikati), anayejenga barabara ya Mwigumbi-Maswa KM 50.3 inayojegwa kwa kiwango cha lami ambao ujenzi wake umefikia takribani asilimia 77.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Mwigumbi, wakati alipokagua ujenzi wa barabara ya Mwigumbi-Maswa KM 50.3 inayojengwa kwa kiwango cha lami.
Muonekano wa sehemu ya Barabara ya Mwigumbi-Maswa KM 50.3 inayojengwa kwa kiwango cha lami mkoani Shinyanga.
Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), mkoa wa Mwanza Eng. Marwa Rubirya (kushoto), akitoa taarifa kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kulia), kuhusu maendeleo yaliyofikiwa ya ujenzi wa barabara ya Usagara-Kisesa KM 16.135 inayojengwa kwa kiwango cha lami mkoani humo

Muonekano wa sehemu ya Barabara ya Usagara-Kisesa KM 16.135 inayojengwa kwa kiwango cha lami mkoani Mwanza.

…………………………………………………………………

Serikali imesema itawalipa fidia kwa mujibu wa sheria wananchi wote waliopisha ujenzi wa barabara katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Amesema hayo Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa wakati akizungumza na wananchi wa Mwigumbi mkoani Shinyanga alipokagua ujenzi wa barabara ya Mwigumbi – Maswa yenye urefu wa KM 50.3 inayojengwa kwa kiwango cha lami na mkandarasi wa Kampuni ya CHICO na kuridhishwa na kasi ya ujenzi wake ambao unagharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 61.

“Kila anayestahili kulipwa fidia atalipwa kama sheria inavyoelekeza na endapo akatokea yeyote mwenye malalamiko Serikali ipo itamsikiliza”, amesema Waziri Prof. Mbarawa.

Amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa Mkandarasi na Viongozi wa Wakala wa Barabara (TANROADS), wa mkoa ili kuhakikisha barabara hiyo inakamilika kwa wakati na spidi inayotakiwa.

Aidha, Waziri Prof. Mbarawa amewahimiza makandarasi wote nchini kutoa kipaumbele cha ajira kwa wakazi wa maeneo husika inapopita miradi ya maendeleo ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali ili kuwapatia kipato na kuinua uchumi wao.

Naye, Kaimu Meneja wa TANROADS mkoa wa Shinyanga Eng. Batholomeo Ndirimbi, amesema mpaka sasa tayari fedha zimetengwa kwa ajili ya ulipaji fidia na watahakikisha kuwa fedha hizo zinalipwa kwa watu sahihi wanaostahili fidia hizo.

“Tutasimamia zoezi hili kwa umakini na kutoa fidia kwa wale wote wanaostahili kisheria”, amesema Eng. Ndirimbi.

Ameongeza kuwa ujenzi wa barabara hiyo umefikiwa asilimia 77 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu.

Katika hatua nyingine, Waziri Prof. Mbarawa amekagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Usagara-Kisesa KM 16.1 inayojengwa kwa kiwango cha lami ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 75 na daraja la Nyashishi lenye urefu wa mita 67.9 ambalo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 99.5 mkoani Mwanza.

Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mwanza Eng. Marwa Rubirya, amesema ujenzi wa barabara hiyo unaendelea vizuri na mkandarasi atamaliza kwa wakati uliopangwa na viwango walivyokubaliana katika mkataba.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad

Responsive Ads Here