AKINAMAMA WALIMA NYANYA KINYEREZI DAR WAJIFUNZA KILIMO CHA UYOGA - JAMII BLOG

Jamii Yetu , Maisha Yetu

Post Top Ad

Responsive Ads Here

Friday 23 June 2017

AKINAMAMA WALIMA NYANYA KINYEREZI DAR WAJIFUNZA KILIMO CHA UYOGA

Mafunzo kwa vitendo. Akinamama wa Kinyerezi Green Voices
wakiweka udongo kwenye mifuko kama maandalizi ya kilimo cha uyoga.

Mafunzo
ya nadharia: Mkufunzi wa kilimo chau yoga wa kikundi cha Bunju Tunza Women, Bi.
Esther Chiombola, akitoa mafunzo kwa wanakikundi wa Kinyerezi Green Voices
waliotembelea mradi wa akinamama wa Bunju kwa nia ya kubadilishana uzoefu.
Mshiriki
kiongozi wa kikundi cha akinamama walima uyoga Bunju, Bi. Magdalena Bukuku,
akimkabidhi Dkt. Sophia Mlote kitabu cha namna ya kulima uyoga.

Mkufunzi
wa kilimo chau yoga, Bi. Esther Chiombola, akiwapatia vipeperushi washiriki wa
mafunzo hayo ya siku moja.
Akinamama
wa kikundi cha Kinyerezi Green Voices wakipita kwenye banda (shamba) la uyoga
walipokwenda hivi karibuni kwa mafunzo ya siku moja ya kubadilishana uzoefu.

AKINAMAMA wanaojishughulisha na kilimo cha nyanya,
spinachi, kabichi na mapapai kutoka Kinyerezi jijini Dar es Salaam wameamua
kujifunza pia kilimo cha uyoga kutoka kwa wenzao wa Bunju ikiwa ni hatua ya
kuongeza fursa ya ujasiriamali pamoja na kubadilishana uzoefu.
Wakiongozwa na Dkt. Sophia Mlote, akinamama hao wa
kikundi cha Kinyerezi Green Voice wameamua kuchukua hatua hiyo katika awamu ya
pili ya kutekeleza Mradi wa Green Voices unaolenga kuwawezesha wanawake
kujihusisha na shughuli za kiuchumi zinazoendana na kukabiliana na mabadiliko
ya tabianchi na uhifadhi wa mazingira.
Ziara hiyo ya mafunzo ya siku moja ilifanyika mwishoni
mwa wiki iliyopita ikiwahusisha akinamama 13 wa kikundi hicho cha Kinyerezi
ambao wanashiriki kilimo hai katika maeneo yao kwa kutumia mabanda maalum
ambapo kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita wameweza kunufaika na bidhaa
wanazozalisha.
Awamu ya pili ya mradi huo wa Green Voices imeanza mwezi
Aprili 2017 na itaishia Aprili 2018, ambapo mradi huo unafadhiliwa na taasisi inayojihusisha na maendeleo ya
wanawake wa Afrika, ijulikanayo kama Foundation for Women of Africa
inayoongozwa na Makamu wa Rais mstaafu wa Hispania, María Teresa Fernández de
la Vega.
Dkt. Mlote alisema kwamba, wameamua kwenda kujifunza
kilimo chau yoga siyo tu katika kubadilishana uzoefu, bali pia kuongeza ujuzi
ili kupata tija katika shughuli za kilimo rafiki wa mazingira katika
utekelezaji wa mradi huo wa Green Voices.
“Tunataka kujifunza aina mbalimbali za kilimo kwa sababu
hii ni fursa nzuri ya kumwezesha mwanamke kujiajiri na kuongeza pato kiuchumi,”
alisema Dkt. Mlote.
Dkt. Mlote, ambaye ni Ofisa Mwandamizi katika Wizara ya
Kilimo, Chakula na Mifugo, alisema mazingira walioyonayo katika kuendesha
kilimo hifadhi cha nyanya, kabichi na mapapai huko Kinyerezi hhayana tofauti na
mazingira ya kilimo cha uyoga kwani shughuli zote zinafanyika katika maeneo
madogo ya nyumba zao huku wakihitaji kiasi kidogo cha maji.
“Ni rahisi kuendesha miradi hii
kwa kuwa shughuli zote zipo nyumbani na hata utarudi usiku kutoka kazini, bado unaweza
kuingia shambani na kuhudumia mimea kwa kutumia mwanga wa taa zilizomo kwenye banda,”
alisema.
Kikundi hicho cha ‘Kinyerezi Green
Voices’ kinaundwa na wanawake 10, ambao baada ya mafunzo walioyoyapata katika
awamu ya kwanza ya mradi wa Green Voices walijikita katika kilimo cha mazao
mbalimbali yakiwemo nyanya, kabichi, pilipili hoho, matango na matikiti maji.
Esther Chiombola ‘Mama Uyoga’,
Ofisa Kilimo Msaidizi Mwandamizi wa Manispaa ya Kinondoni ndiye mkufunzi wa
kikundi cha ‘Bunju Tunza Women Group’ kinachojihusisha na kilimo cha uyoga, ambaye
allitumia muda mwingi kuwaelimisha akinamama wa Kinyerezi kuelezea umuhimu wa
kilimo chau yoga pamoja na faida zake.
Alisema uyoga ni lishe bora iliyojaa
kiasi cha asilimia 20 hadi 49 cha protini pamoja na Vitamini B, C, D, E, na K,
na madini joto, chuma, fosforas, potashi, zinki na shaba na kwamba hauna lehemu
(cholesterol).
Alisema baadhi ya aina za uyoga
kama Ganoderma husaidia kuzuia na kupunguza kasi ya magonjwa sugu kama
saratani, kisukari, kifua kikuu, moyo, shinikizo la damu na figo.
“Kilimo cha uyoga ni ajira
kubwa kwa akinamama, vijana, wazee na wastaafu na ni kilimo rafiki
kinachopunguza uchafuzi wa mazingira kwa vile kinatumia mabaki ya shambani na
viwandani,” alisema na kuongeza kwamba kilimo hicho ni endelevu ambacho hakina
msimu.
Bi. Magdalena Bukuku ni mshiriki kiongozi wa Bunju Tunza
Women Group ambaye alisema kwamba, tangu walipoanzisha mradi huo mwaka 2016
akinamama wameweza kunufaika na kuongeza mapato kutokana na bidhaa zao kupata
soko kubwa katika maeneo mengi ya jijini Dar es Salaam.
“Hata kwenye maduka makubwa (super markets) wamekuwa
wakiuhitaji kwa ajili ya wateja, hivyo soko la uhakika lipo la kutosha,”
alisema Bi. Magdalena.
Aidha, aliongeza kwamba, kikundi chao kimekuwa kama darasa
kwani watu wengi, wanawake kwa wanaume, kutoka mikoa ya Tanzania Bara na
Zanzibar wamekuwa wakienda kujifunza kila mara kuhusu kilimo hicho.
“Ni mradi mzuri, unatumia gharama kidogo huku mavuno yake
yakiwa endelevu hasa ukiwa na nia, dhamira na jitihada, soko lake lipo kubwa,”
alieleza Magdalena.
Dkt. Mlote na Bi. Magdalena Bukuku ni miongoni mwa
akinamama 15 wanaotekeleza Mradi wa Green Voices nchini Tanzania baada ya
kupatiwa mafunzo nchini Hispania mwaka 2016 ambapo lengo ni kupaza sauti za
wanawake kwa ajili ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi kwa kushiriki
shughuli za kilimo rafiki wa mazingira.
Akinamama wengine wanatekeleza
miradi mbalimbali ya ujasiriamali unaoendana na mapambano dhidi ya mabadiliko
ya tabianchi katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Kigoma, Kilimanjaro,
Pwani na Mwanza.
Mratibu wa mradi wa Green Voices nchini Tanzania, Bi. Secelela Balisidya,
alisema katika awamu ya pili, mbali ya akinamama hao kuendeleza miradi yao ya
awali, pia watapata fursa ya kubadilisha uzoefu na kuona uwezekano wa
kutekeleza mmiradi mingine tofauti kwa faida yao.
huo wa kilimo hai cha nyanya kwa kutumia green house ni sehemu ya miradi
10 inayoendeshwa nchini Tanzania kupitia Green Voices ambapo inaendeshwa katika
mikoa sita ya Tanzania Bara.
Mikoa hiyo ni Dar es Salaam,
Pwani, Mwanza, Kigoma, Morogoro na Kilimanjaro ambapo inahusisha kilimo,
usindikaji, ufugaji na utafiti.
“Jumla kuna miradi 10 ikiwemo
ya kilimo cha miti ya matunda mkoani Kigoma, kilimo cha viazi lishe visiwani
Ukerewe mkoani Mwanza, Ufugaji Nyuki mkoani Morogoro na Pwani, ukaushaji wa
mbogamboga kwa kutumia nishati ya jua mkoani Morogoro, usindikaji wa vyakula
mbalimbali kutokana na muhogo mkoani Pwani, kilimo hai cha mbogamboga, kilimo
cha uyoga mkoani Dar es Salaam, mradi wa majiko banifu mkoani Pwani na mradi wa
utafiti wa jiko linalotumia nishati ya jua mkoani Kilimanajro,” alifafanua
Secelela Balisidya.
Aidha, alisema, lengo kubwa la
mradi wa Green Voices ni kupaza sauti za akinamama kueneza ujuzi wao wa
kupambana na mabadiliko ya tabianchi ili jamii nzima ya Kitanzania iweze
kujifunza zaidi na kuzitumia mbinu hizo katika kupambana na mabadiliko ya
tabianchi.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad

Responsive Ads Here