Mradi mkubwa wa kijiji cha digitali cha Ololosokwan, Loliondo umezinduliwa rasmi mwishoni mwa wiki, miaka miwili tangu kutiwa saini kwa uanzishwaji wake kati ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) na kampuni ya Samsung.
Hiki kitakuwa ni kijiji cha nne cha digitali barani Afrika cha kwanza kikiwa nchini Afrika Kusini huku kingine kikiwa Gabon na Ethiopia.
Kijiji hicho cha digitali ni nadharia ya Samsung katika kurejesha faida kwa umma na kina huduma mbalimbali ambazo zikiunganishwa na haja ya wananchi zitasaidia kubadili maisha ya wamasai na kuondokana na utegemezi wa mifugo pekee.
Uzinduzi rasmi wa kijiji hicho umefanywa na Mkuu wa mkoa Arusha Mrisho Gambo kwa niaba yaWaziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na watoto Ummy Mwalimu.
Kijiji hicho cha digitali kina shule yenye tehama ikiwa na maunganisho ya intaneti, kiliniki ya kisasa ikiwa na kituo cha teknolojia ya mawasiliano yenye kuwezesha utabibu (telemedicine) na jenereta linalotumia nguvu za jua.
Mradi huo ambao ulishuhudiwa utiaji saini na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya UNESCO, Bi. Leah Kihimbi kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na Dkt. N. Iriya kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) Dar es Salaam na wafanyakazi wa UNESCO mwaka 2014, kukamilika kwake kunawezesha UNESCO na serikali ya Tanzania kuwapatia wakazi wa eneo hilo huduma bora za afya na vijana wa Kimasai nafasi ya kupata elimu kutokana na ukweli kuwa kwa utamaduni na kazi zao za ufugaji wamekuwa wakipata shida ya kupata elimu.
Utiaji saini wake katika mwaka huo ulifanywa na Mkuu wa ofisi na Mwakilishi Shirika la UNESCO nchini Bi. Zulmira Rodrigues na Mkurugenzi wa Samsung Electronics nchini Tanzania, Bw. Mike Seo .Kupitia kijiji hicho vijana wataendelea na masomo hata kama wanachunga mifugo yao kutokana na kupatiwa tablet ambazo zitawawezesha kujifunza hata wakiwa nje wakichunga mifugo yao.
Aidha miongoni mwa manufaa makubwa yatakayopatikana katika mradi huo wa kijiji cha digitali ni kuweza kupata nishati rahisi na iliyo rafiki kwa mazingira kwa kuwepo na jenereta linalotumia nishati ya jua.Kuwepo kwa kijiji hicho kunataka kudhihirisha ni kwa namna gani teknolojia inaweza kutumika kuleta mabadiliko chanya yanayotakiwa kwa ajili ya maendeleo ya wananchi waliopo vijijini.
Kijiji hicho cha Loliondo ambacho kitakuwa cha nne katika vijiji vya kidigitali barani Afrika kimeelezwa naMkuu wa mkoa wa Arusha Mheshimiwa Mrisho Gambo kama utekelezaji wa Sera ya Tiba Mtandao kutokana na kuzinduliwa kwa Kliniki Mtandao iliyopo katika Kijiji hicho.Katika uzinduzi wa mradi huo kwa ujumla wake, kliniki ndicho kitu ambacho kinaonekana kwenda karibu zaidi na wananchi wa Ololosokwan kwani itakuwa inatoa huduma za afya, bora za kisiasa na za haraka kwa wakazi wa kata za Soitsambu naa Oloipiri, Wilayani Ngorongoro.
Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa mkoa wa Arusha ,Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, wazee na watoto Mhe Ummi Mwalimu wakati wa uzinduzi wa kliniki hiyo,alisema kuwa Tiba Mtandao imekua ni miongoni mwa Vipaumbele vya Wizara yake ili wananchi wote Tanzania waweze kupata huduma stahiki za matibabu pasipo kujali changamoto za Kijiografia zinazotukabili,
Pamoja na kufanya uzinduzi huo katika hotuba yake Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo aliwashukuru wote walioshiriki kuleta Mradi huo wa maana kwa mkoa wa Arusha kwani wangeweza kupeleka sehemu nyingine yeyote na kuongeza kuwa ni deni kubwa sana lazima tuhakikishe huduma hiyo imefanikiwa.
Akizungumzia masuala ya afya kama kipaumbele katika mradi huo wenye lengo la kuhifadhi utamaduni wa kimasai huku wakitumia teknolojia ya kisasa kuleta maendeleo katika elimu na kuhifadhi mazingira, Mkuu huyo wa mkoa akizungumza kwa niaba ya Waziri alisema kuwa kutokana na umuhimu wa sekta ya afya kwa kila Mtanzania ,serikali itaelekeza nguvu katika Kliniki hiyo ili kuiwezesha kutoa huduma stahiki na Kwa muda mrefu kwa wananchi wa maeneo haya.
"Kliniki hii ni ya kwanza Tanzania na itaweza kutoa huduma bora na za kisasa kwa njia ya mtandao kwa wananchi zaidi ya elfu kumi kutoka katika maeneo ambayo hapo awali wananchi walikuwa wanatembea umbali mrefu zaidi ya Kilomita 50 kufuata huduma za afya".
" Hii inadhihirisha kwamba mwananchi wa Ololosokwan na maeneo ya jirani anaweza kuhudumiwa na daktari bingwa aliyeko Muhimbili au kokote Duniani kupitia Klinik hii;na mfumo wa Mtandao uliopo unaruhusu upatikanaji wa huduma hizi kwa kipindi chote cha mwaka mzima".
Aidha aliitaka Halmashauri kutenga Bajeti kwa ajili ya kuongeza hadhi ya zahanati hiyo kuwa Kituo cha Afya ambapo itaenda sambamba na kuongeza majengo Pamoja na wataalam watakaoweza kutoa huduma stahiki Kwa wananchi.
Upatikanaji wa kituo cha Afya katika eneo hilo huku kukiwepo na kliniki mtandao kutasaidia kuokoa maisha ya wananchi ambao wengi wao waliamini kupona magonjwa makubwa ni mpaka uende KCMC au Muhimbili tu.
Awali akizungumza katika uzinduzi huo Mkuu Shirika la Umoja wa mataifa linaloshigulikia Elimu na Sayansi (UNESCO) nchini Tanzania Bi. Zulmira Rodrigues alisema kijiji hicho ni ushuhuda tosha wa ukuaji wa teknolojia unaenda sambamba na maono ya shirika la Unesco la kutoa kipaumbele katika miradi ya sayansi inayosaidia wananchi wenye mahitaji moja kwa moja.
Alisema kwa kutambua adha waliyokuwa wanaipata wananchi wa Ololosokwan walitengeneza mradi ambao sehemu mojawapo ni kliniki Mtandao ili kuleta mabadiliko ya afya za watu kwa njia ya kisayansi.
Naye mkurugenzi wa Tiba Kutoka Wizara ya Afya Dr. Margareth Evelyne Mhando alishukuru Unesco kusaidia kutekeleza malengo ya Wizara kupitia Mradi huu wa kijiji cha digitali na kuongeza kuwa ni hatua nzuri katika sekta ya afya Kwa sababu hivi sasa wananchi waliombali na vituo vya Afya kupitia Mradi huu watapata huduma bora kutoka Kwa matabibu wabobezi.
Uzinduzi wa Mradi huu ulihudhuriwa pia na Balozi wa Switzerland Nchini Tanzania Bi. Florence Mattli, Wawakilishi wa Samsung ambao ndio waliotoa fedha na Teknolojia pamoja na wawakilishi kutoka Umoja wa Ulaya (EU).
Bi. Mattli alisema kwamba wataendelea kusaka wadau wengine kuhakikisha kwamba mradi huo unaendelea kutanuka na kufanikiwa kwa kujazia maeneo ambapo panahitaji nguvu nyingine.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mh. Mrisho Gambo akifanya kipimo cha B.M.I ndani ya kituo cha huduma maalum za afya kilichopo katika kijiji cha Ololosokwan, wilayani Ngorongoro mkoani Arusha mara baada ya kukizundua rasmi.
No comments:
Post a Comment