SERIKALI KUTOA MAFUNZO MAALUM KWA MABLOGA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2025 - PAMWASH BLOG

Jamii Yetu , Maisha Yetu

Tuesday, 15 July 2025

SERIKALI KUTOA MAFUNZO MAALUM KWA MABLOGA KUELEKEA UCHAGUZI MKUU 2025



Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam 

Serikali imetangaza mpango wa kutoa mafunzo maalum kwa waandishi wa blogu nchini, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2025. Mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha mabloga kusambaza habari sahihi, zenye weledi na zinazozingatia maadili ya uandishi wa habari katika kipindi hicho muhimu cha kidemokrasia.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, wakati wa Mkutano wa Wadau wa Sekta ya Habari uliofanyika Julai 9, 2025 katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Katika mkutano huo, uliojadili mchango wa sekta ya habari katika kufanikisha Uchaguzi Mkuu wa 2025, Mwenyekiti wa Chama cha Mabloga Tanzania (TBN), Beda Msimbe, alitoa wito kwa serikali kuangalia umuhimu wa kuwafundisha mabloga wengi ambao, japo si waandishi wa habari kitaaluma, wanazalisha maudhui yenye ushawishi mkubwa katika jamii.

"Wapo wengi wanaotengeneza maudhui, na baadhi yao si waandishi wa habari. Hawa wanahitaji mafunzo ili waelewe namna ya kuandika habari za kisiasa kwa weledi kuelekea uchaguzi mkuu," alisema Msimbe.


Alisisitiza kuwa katika zama za sasa za teknolojia na matumizi ya akili bandia (AI), blogu na tovuti zimebeba jukumu kubwa zaidi la kuwa vyanzo vya habari vinavyoaminika kuliko mitandao ya kijamii, hivyo kuhitaji maboresho ya weledi kwa watengeneza maudhui.

Msimbe aliipongeza serikali kwa kuandaa mkutano huo wa wadau, akisema ni hatua chanya kuelekea uchaguzi wa haki na uwazi, licha ya changamoto ya mada nyingi kujadiliwa kwa siku moja.

Akijibu hoja hiyo, Katibu Mkuu Gerson Msigwa aliagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuandaa mafunzo hayo kwa haraka ili kuwajengea uwezo mabloga kabla ya uchaguzi.

Hatua hiyo imepokelewa kwa pongezi na wadau mbalimbali wa habari, wakitafsiri kuwa ni ishara ya kutambuliwa rasmi kwa mchango wa mabloga katika mchakato wa kidemokrasia na maendeleo ya tasnia ya habari.

Chama cha Mabloga Tanzania (TBN) kina wanachama zaidi ya 200 waliotawanyika ndani na nje ya nchi. Mafunzo hayo yanatarajiwa kuwa na athari chanya katika kuhakikisha habari zinazotolewa kipindi cha uchaguzi zinakuwa za kitaaluma, sahihi na zenye kuzingatia maadili ya taaluma ya habari.

Mkutano huo ulifunguliwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, ambaye alisisitiza umuhimu wa vyombo vya habari na taasisi za usalama kushirikiana katika kudumisha amani na uvumilivu wakati wa mchakato wa uchaguzi.

No comments:

Post a Comment

HABARI