WATOTO WATAKIWA KUTOA TAARIFA ENDAPO WAKIONA DALILI ZA KUFANYIWA UKATILI - JAMII BLOG

Jamii Yetu , Maisha Yetu

Post Top Ad

Responsive Ads Here

Thursday, 12 October 2017

WATOTO WATAKIWA KUTOA TAARIFA ENDAPO WAKIONA DALILI ZA KUFANYIWA UKATILI

 
Watoto wametakiwa kutambua kuwa ni wajibu wao kutoa taarifa kwa walimu wanaowaamini pindi wanapohisi au wanapoona dalili na zaidi wanapofanyiwa vitendo vya ukatili na wazazi, walezi na jamii zao ikiwemo kukeketwa, mimba na ndoa za utotoni.
 
Rai hiyo imetolewa na wadau wa Watoto kutoka shirika la Ace Africa na Center for Women and Children Development (CWCD) wakati wa maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Kike duniani yaliyofanyika kwenye shule ya Msingi Engalaoni kata ya Mwandeti halmashauri ya Arusha kwa kuwataka watoto kujilinda wao kwanza dhidi ya Ukatili wa  watoto licha ya kuwa jamii inajukumu la kuwalinda. 
 
Petro Laizer wa shirika la CWCD amesema kuwa licha ya mtoto kufahamu haki zake dhidi ya ukatili wa mtoto lakini pia watoto wana wajibu mkubwa wa kutambua kuwa wanatakiwa kujilinda kwanza na kutoa taarifa kwa walimu pale wanapohisi au kufanyiwa ukatili ikiwepo kukeketwa, kuchumbiwa, kuzuiwa kwenda shule pamoja na kulawitiwa.
 
Amefafanua kuwa watoto wasitegemee ulinzi wa wazazi peke yake bali watambue kuwa wao ni walinzi namba moja dhidi ya ukatili unaofanywa na wazazi na jamii zao kwa kuwa watoto wengi walikuwa hawajui kama wanapaswa kujilinda kwanza.
 
"Watoto wanafanyiwa ukatili mkubwa ndani ya familia na jamii zao kama shirika tumewajengea uwezo na kuwawekea mazingira salama ya kutoa taarifa kwa walimu maalumu kwenye shule zao na wale wanaowaamini zaidi" amesema Petro
 
Hata hivyo watoto wa kike wamethibitisha kuchukizwa na kitendo cha wazazi wao kuwakeketa, kuwaoza katika umri mdogo pamoja na watoto wakike kupelekwa kuchunga ng'ombe badala ya kwenda shule.
 
Nipael Melinyo amesema kuwa wanachukizwa na ukatili wanaofanyiwa watoto katika jamii yao na kuthibitisha kuwa yuko tayari kutoa taarifa akihisi kuna maandalizi ya kukeketwa ama kuchumbiwa si kwake pekee hata kwa mtoto wa jirani.
 
Amesema kuwa amefurahishwa sana na mafunzo ya siku ya mtoto wa kike yamempa ufahamu wa kuwa anaweza kutoa taarifa ya matukio ya ukatili kwa watoto ambapo awali hakufahamu kama ana wajibu wa kutoa taarifa  hata kwa mwalimu dhidi ya mila na desturi za jamii yao.
 
Namayani Joseph ameiomba serikali kuwasaidia watoto wote kupata haki zao  kwani kwenye jamii yao hata kwa watoto wa kiume wananyimwa haki kwa kuzuiwa kwenda shule na badala yake wanapelekwa kuchunga ng'ombe.
 
Suzana mwanafunzi wa darasa la sita shule ya Msingi Olbaki mwenye ndoto ya kuwa mwalimu amewaomba wazazi wasimuoze angali mdogo na wamuache asome ili atimize ndoto yake na kudhihirisha wazi kuwa hatakubali jambo hilo na yuko tayari kutoa taarifa endapo atahisi wazazi wake kupokea sukari ya uchumba.
 
"Ninawaomba wazazi waniache nisome ninataka kuwa mwalimu na sitakubali wazazi wangu kunilazimisha kuolewa nikiwa mtoto nitatoa taarifa kwa mwalimu endapo watafanya hivyo"amesisitiza Suzana
 
Mwalimu mkuu shule ya msingi Engalaoni mwalimu Ester Kimaro amesema kuwa licha ya kufurahishwa na maadhimisho hayo bado kuna changamoto kubwa katika jamii ikiwa ni pamoja na kukeketwa, watoto kuchumbiwa wangalia shuleni na wengine kupelekwa kuchunga ng'ombe 
 
"Ukizungumza na watoto wenyewe hawataki kuolewa ila tatizo kubwa ni uelewa mdogo wa jamii unaotokana na mila na desturi kunakua na mgogoro baina ya wazazi, utakuta baba anataka mtoto aolewe mama hataki, pengine mama anataka baba hataki na wakati mwingine wazazi wote hawataki lakini kutokana na mila jamii inawalazimisha kupokea sukari na wanakubali kwa kuhofia kutengwa na jamii" amesema mwalimu Mkuu huyo
 
Mwalimu Kimaro ameelezea kuwa tayari tumeanzisha za klabu za watoto kwa ajili ya kujengewa uwezo wa kutambua haki na wajibu wao, na kuweka siku maalumu za kuzungumza na wazazi shuleni pamoja na kushirikiana na uongozi wa kijiji kuelimisha jamii juu ya madhar ya ukatili kwa watoto.
 
Awali maadhimisho hayo yalianza na maandamano yaliyofanywa na watoto wa kike wakiwa wamebeba vibao vyeny jumbe mbalimbali za kupiga vita Ndoa za Utotoni na watoto wakionyesha kuomnpba wazazi wawache wasome pamoja na shirika la Ace Africa kugawa nguo za ndani na sodo kwa watoto hao.
 
Siku hiyo ya Mtoto wa Kike imeadhimishwa ikiwa na changamoto kubwa ya watoto wa kike kukeketwa na ndoa za utotoni ambapo tafiti zinaonyesha watoto wengi  wamechumbiwa wakiwa bado wanasoma na ni kiashiria tosha kwamba sio rahisi mtoto aliyechumbiwa kusubiriwa mpaka afikie malengo nibdhahiri atakatishwa ndoto zake siku yoyote.
 
Jamii inatakiwa kuchukua hatua za ziada za kuwalinda watoto pamoja na kutoa taarifa kwa vyombo husika kwa yeyote atakayejihusisha na vitendo vya ukatili huo kwa watoto.
 
 
 
 
PICHA ZA MATUKIO YA SIKU YA MTOTO WA KIKE DUNIANI SHULE YA MSINGI ENGALAONI.



 

 



CHANZO:http://msumbanews.com/watoto-wametakiwa-kutoa-taarifa-wanapoona-dalili-za-kufanyiwa-vitendo-vya-ukatili/

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad

Responsive Ads Here