Na Hamza Temba - WMU - Muheza, Tanga
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani ameuagiza uongozi wa Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga kukutana na wakulima 879 wa vijiji vitano katika Tarafa ya Amani Wilayani humo kwa ajili kufanya uhakiki wa malipo ya fidia ya mazao waliyolipwa na Serikali ili kupisha eneo la hifadhi ya msitu wa Derema.
Mhandisi Makani ametoa agizo hilo jana katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Msasa IBC, Tarafa ya Amani, Wilayani Muheza kufuatia malalamiko ya wananchi hao kupunjwa malipo yao wakati wa ziara yake ya siku moja wilayani humo kwa ajili kutatua mgogoro wa ardhi uliodumu kwa zaidi ya miaka 15 baina Serikali na wananchi wa vijiji hivyo vya Kisiwani, Kwemdim, Msasa IBC, Antakae na Kambi.
Akisoma risala ya wakulima hao mbele ya Naibu Waziri Makani, Mwenyekiti wa Kamati ya wakulima hao, Mohammed Rama Shesha alidai kuwa jumla ya wakulima 1,128 wa vijiji hivyo wanailalamikia Serikali kwa kuwalipa viwango pungufu vya malipo ya fidia ya mazao yao tofauti na viwango vilivyolipwa na Serikali mwaka 2002 kupitia mradi wa FINIDA. Aidha, alidai kuwa kuna baadhi ya mazao pia hayakulipiwa kabisa fidia hizo.
Akizungumzia viwango vya fidia hizo Shesha alisema wananchi walilipwa Shilingi 28,800 kwa mche mmoja wa iliki na Shilingi 11,000 kwa mche mmoja wa mgomba. Alidai viwango hivyo vilibadilika kuanzia mwaka 2005 ambapo walilipwa Shilingi 3,315 kwa kila mche mmoja badala ya Shilingi 5,100 kama ilivyoainishwa kwenye viwango vya Serikali hivyo akaomba walipwe kiasi kilichobakia cha shilingi 1,785.
Akitolea ufafanuzi wa malalamiko hayo, Naibu Waziri Makani alisema idadi kamili ya wananchi waliohakikiwa katika eneo hilo ni 879 na sio 1,128 kama alivyodai mwenyekiti huyo. Aidha, alisema viwango vilivyotumiwa kuwalipa wananchi hao mwaka 2002 sio vya Serikali na kwamba vilitumiwa na mradi wa FINIDA uliofadhiliwa na Serikali ya Finland kwa ajili ya kulipa fidia wananchi wa mpakani na hifadhi hiyo ili kufanikisha zoezi la kuanisha mpaka wa hifadhi hiyo na kusaidia Serikali kutimiza azma ya kuhifadhi eneo hilo.
Alisema viwango halali vya Serikali vilivyopo kisheria kwa ajili ya kulipa fidia ya mimea hiyo ni kuanzia Shilingi 5,100 kwa kiwango cha juu kwa mmea uliokoma kufikia kiwango cha uzalishaji, Shilingi 3,315 kwa mmea wenye mwaka mmoja na Shilingi 2,040 kwa mmea wenye mwezi mmoja. Alisema viwango vingine vya malipo kwa kiwango cha chini ni Shilingi 204, Shilingi 102 na Shilingi 51.
Alisema Serikali iliamua kulipa kiwango cha Shilingi 3,315 kwa mazao yote ikiwemo yale yaliyostahili kulipwa kiwango cha chini kabisa cha Shilingi 51 ili kuweka uwiano na kurahisha zoezi hilo la malipo. Alihoji kama kuna mwananchi yeyote aliyelipwa chini ya kiwango hicho japokuwa kulikuwepo na wengine mazao yao yalistahili kulipiwa viwango hivyo, hakuna aliyejitokeza.
Kufuatia ufafanuzi huo aliuagiza uongozi wa Wilaya ya Muheza kutumia kipindi cha mwezi mmoja kuanzia leo Jumatatu kuonana na wakulima hao ili kuhakiki malipo yao na hatua zaidi ziweze kuchukuliwa kama kuna yeyote aliyezulumiwa apewe haki yake.
"Kwa wale ambao tayari wana kumbukumbu zao vizuri wazilete mbele ya Serikali, kupitia wao pengine tunaweza kupata picha ya jumla pengine kulikua na mapungufu kwenye malipo. Kuanzia jumatatu ijayo Mhe. DC tulitekeleze hilo la kukusanya nyaraka kwa wale walizonazo tuweze kuzilinganisha na zile tulizokua nazo Serikalini tujadiliane nao kwamba ni kitu gani kimebaki tofauti katika maeneo yale yale mliyofanyiwa uhakiki", alisema Mhandisi Makani.
Alisema kwa wale ambao wamepoteza nyaraka zao za malipo wataandaliwa utaratibu maalum wa uhakiki kwa kuwa kumbukumbu zote za malipo zipo kwenye Kompyuta za halmashauri ya Wilaya ya Muheza.
Alisema lengo la Serikali ya awamu ya tano ni kuhakikisha inamaliza kabisa migogoro ya ardhi nchini. “Tutahakikisha tunaboresha zaidi usimamizi wa uhifadhi wa rasilimali zetu za misitu, wanyamapori na nyinginezo kuhakikisha migogoro hiyo inapungua kwa kasi kuelekea kwenye sifuri, zero rate", alisema Makani.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mwanaisha Tumbo alisema, Serikali ya Wilaya imepokea maelekezo hayo na itayafanyia kazi na kwamba maafisa wa Halmashauri watafika katika kila kijiji siku ya Jumatatu na Jumatano kwa ajili ya kuendesha zoezi hilo la uhakiki.
Akizungumzia zoezi la fidia Mkuu huyo wa Wilaya alisema pamoja na wananchi hao kulipwa fidia za mazao yao ambayo yalilipwa kwa awamu tatu, asilimia 50 mwaka 2005, asilimia 25 mwaka 2006 na asilimia 25 mwaka 2008, pamoja na asilimia 23 kama fidia ya ucheleweshaji wa deni, Serikali pia itawapa maeneo ya fidia ambapo kila mwananchi aliyeathirika eneo lake atapewa ekari tatu.
Alisema eneo ambalo limeanishwa kwa ajili ya kuwagawia wananchi hao ni lililokuwa shamba la mkonge Kibaranga ambalo lina ukubwa wa hekta 1370 sawa na ekari 3425 na lilikua likimilikiwa na Bodi ya Mkonge, eneo hilo lilitolewa tamko ya kufutiwa umiliki wake na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli mwezi Julai, 2016.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani (katikati), akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Msasa IBC wilaya ya Muheza mkoani Tanga jana wakati wa ziara yake ya siku moja wilayani humo kwa ajili kutatua mgogoro wa hifadhi ya msitu wa Derema. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mwanaisha Tumbo.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani (katikati), akimuonesha mwenyekiti wa kamati ya wakulima wa vijiji vitano vya tarafa ya Amani, Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga, Mohammed Ramadhani Shesha viwango halali vya serikali vya kulipia fidia za mazao kwa wananchi waliondolewa katika eneo la hifadhi ya msitu wa Derema wakati wa ziara yake ya siku moja wilayani humo jana kwa ajili ya kutatua migogoro wa hifadhi hiyo. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Mwanaisha Tumbo.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani (kulia), akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Msasa IBC wilaya ya Muheza mkoani Tanga jana wakati wa ziara yake ya siku moja wilayani humo kwa ajili kutatua mgogoro wa hifadhi ya msitu wa Derema.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani, (wa tatu kushoto), akiangalia eneo la Msitu wa hifadhi ya Derema na viongozi wa wilaya ya Muheza Muheza wakati wa ziara yake ya siku moja wilayani humo jana kwa ajili ya kutatua mgogoro wa hifadhi hiyo.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani (kulia), akisalimiana na wananchi wa Kijiji cha Msasa IBC wilaya ya Muheza Mkoani Tanga jana wakati wa ziara yake ya siku moja wilayani humo kwa ajili ya kutatua mgogoro ya hifadhi ya msitu wa Derema.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani (kushoto), akimuonesha mwenyekiti wa kamati ya wakulima wa vijiji vitano vya tarafa ya Amani, Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga, Mohammed Ramadhani Shesha (kulia) viwango halali vya serikali vya kulipia fidia za mazao kwa wananchi waliondolewa katika eneo la hifadhi ya msitu wa Derema wakati wa ziara yake ya siku moja wilayani humo jana kwa ajili ya kutatua migogoro wa hifadhi hiyo.
No comments:
Post a Comment