FARIDA MANGUBE, MOROGORO
Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA) imekabidhi dawa, vifaa tiba na vitendanishi vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 19 kwa magereza ya mkoa wa Morogoro.
Dawa hizo zimetolewa baada ya msako mkubwa uliofanywa na TMDA Kanda ya Kati katika mikoa ya Dodoma, Iringa, Singida na Morogoro, ambapo ziliondolewa sokoni kwa kutokidhi vigezo vya kanuni ya TMDA ya mwaka 2015.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano, Meneja wa TMDA Kanda ya Kati, Sonia Henry Mkumba, alisema dawa hizo ni salama na bora kwa matumizi ya binadamu na zimekabidhiwa kwa magereza ili zitumike katika vituo vya afya vilivyo chini ya magereza ya mkoa huo.
Mkumba alifafanua kuwa dawa na vifaa tiba hivyo vilipatikana baada ya mamlaka hiyo kufanya ukaguzi na kuondoa dawa zilizouzwa katika maduka yasiyo na vibali vya kutunza na kukuza dawa kwa mujibu wa kanuni za TMDA za mwaka 2015 na marekebisho yake ya mwaka 2018.
Kwa upande wake, Afisa Mnadhimu wa Magereza Mkoa wa Morogoro, ACP Godfrey Boniface Kavishe, aliishukuru TMDA kwa msaada huo, akibainisha kuwa dawa hizo zitakuwa na mchango mkubwa katika utoaji wa huduma za afya kwa jamii ya magereza.
"Dawa hizi zitagawiwa katika vituo 13 vya afya vya magereza mkoani Morogoro, na tunahakikisha kuwa zitatumika ipasavyo kwa mujibu wa miongozo ya afya," alisema ACP Kavishe.
Hatua hii ni sehemu ya jitihada za TMDA kuhakikisha kuwa dawa zinazosambazwa kwa wananchi zinakidhi viwango vya ubora na usalama, sambamba na kudhibiti usambazaji wa dawa zisizo na vibali katika soko la Tanzania.
No comments:
Post a Comment