DKT NCHIMBI AWAPONGEZA WANA GHALUNYANGU KWA UZALENDO WA KUJITOLEA KATIKA MIRADI YA MAJI - JAMII BLOG

Jamii Yetu , Maisha Yetu

Post Top Ad

Responsive Ads Here

Friday, 14 July 2017

DKT NCHIMBI AWAPONGEZA WANA GHALUNYANGU KWA UZALENDO WA KUJITOLEA KATIKA MIRADI YA MAJI




Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi amewapongeza wana kijiji cha Ghalunyangu kilichopo kata ya Makuro Wilayani Singida kwa uzalendo wa kujitolea nguvu kazi ya kuchimba mtaro wenye urefu wa mita 670 katika mradi wa maji kijijini hapo.
Dkt Nchimbi ametoa pongezi hizo mara baada ya kushuhudia mtaro huo utakaopitisha maji kutoka katika chanzo cha maji hadi katika tenki la ukubwa wa lita elfu 10 na kuelekea katika vituo vitatu vya kuchotea maji ikiwa ni jitihada za kufanikisha ukarabati wa mradi wa maji kijijini hapo.
Amesema “nguvu ya kuchimba mtaro huu haitaenda bure, tuna uhakika maji yatafika katika vituo hivyo vitatu kwa kuanzia ili kuwaepusha kuendelea kuchota maji katika bomba moja lililopo eneo la chanzo cha maji”.
Dkt Nchimbi ameongeza kuwa, “uzalendo huu usiishie kwenye kuchimba mtaro tu, nawaomba mtoe ushauri na mapendekezo ili ukarabati wa mradi huu uwe wa ufanisi mkubwa, na hata mkiona mambo yanaenda ndivyo sivyo toeni taarifa mapema, lakini nina imani na halmashauri ya Singida, itatekeleza kwa ufanisi mradi huu kwa manufaa yenu wana Ghalunyangu”.
Aidha amewataka wana kijiji hao kuwa walinzi wa miundo mbinu ya mradi huo pamoja na kutunza chanzo cha maji hasa kwa kuongeza eneo la hifadhi ya chanzo cha maji kutoka mita 60 mpaka mita 100 na kupanda miti ya kutosha katika chanzo hicho.
Kwa upande wake Mhandisi wa Maji wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida Edward Kisalu amesema ukarabati wa mradi huo wa maji unatokana na fedha za malipo kwa matokeo jumla ya shilingi milioni 37 walizopatiwa kutokana na kutekeleza vizuri miradi ya maji Wilayani humo.
Kisalu amesema halmashauri iliamua kutumia fedha hizo kukarabati mradi wa maji katika kijiji hicho kwa kuwa ni mradi pekee ambao unahudumia wakazi zaidi ya elfu mbili huku ukiwa umechakaa kutokana na mashine ya kusukuma maji ya mradi huo kuwa na zaidi ya miaka kumi toka inunuliwe.
Amesema fedha hizo zitatumika kununua mashine mpya ya kusukuma maji, kununua tenki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita elfu 10, ujenzi wa mnara wa kuhifadhia tenki, mabomba ya kupitishia maji pamoja na ujenzi wa vituo vitatu vya kuchotea maji.
Kisalu amefafanua kuwa kutokana na fedha hizo kutotosheleza kukamilisha kazi zote ikiwemo uchimbaji wa mitaro wanakijiji waliamua kwa pamoja wajitolee nguvu kazi zao kuchimba mtaro huo bila malipo yoyote ili ukarabati wa mradi ufanikiwe kwa uharaka zaidi.
Ameongeza kuwa licha ya kuwepo kwa tanki lenye ujazo wa lita elfu 90 kijijini hapo, mabomba ya kupeleka maji katika tanki hilo yamekatika hivyo halmashauri kwenye bajeti ya mwaka 2017/2018 imetenga shilingi milioni 300 za ukarabati mkubwa wa kupeleka maji katika tenki hilo na kuongeza vituo vya kuchotea maji hivyo kufuta kabisa kero ya maji kijijini hapo.
Kwa upande wao wanakijiji cha Ghalunyangu wamempongeza Dkt Rehema Nchimbi kwani amekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kwanza kufika kijijini hapo hali iliyowapa faraja kubwa na ari zaidi ya kujitolea katika miradi ya maendeleo.
Wanakijiji hao licha ya kuwa na itikadi tofauti za kichama kwa kauli moja wamesema wana imani kubwa sana na serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dkt John Pombe Magufuli kwakuwa matokeo chanya yanaonekana na sio maneno tu.
Wamesema wana imani na Rais Magufuli sio tu kwenye miradi ya maji kuwa itatekelezwa vizuri bali hata miradi mingine ikiwa ni pamoja na miundombinu ya barabara ambayo tayari mkandarasi ameanza kazi ya ukarabati wa barabara kijijini hapo.
Naye Mhandisi wa Maji Mkoa wa Singida Mhandisi Lydia Joseph amesema kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2016/17 halmashauri tatu kati ya saba Mkoani Singida zimepokea fedha za malipo kwa matokeo ambapo halmashauri hizo ni Mkalama, Manyoni na Halmashauri ya Wilaya ya Singida.
Mhandisi Lydia amesema halmashauri hizo zimepata fedha hizo kutokana na kazi nzuri ya kuwasilisha taarifa za miradi ya maji kwa wakati na mfululizo hivyo Serikali kupitia Wizara ya Maji na Umwagiliaji imezipatia fedha hizo kama motisha.
Ameongeza kuwa halmashauri ya Wilaya ya Manyoni imepatiwa shilingi milioni 16.6, halmashauri ya wilaya ya Mkalama shilingi milioni 20.1 na halmashauri ya wilaya ya Singida shilingi milioni 37.8.
Aidha Mhandisi Lydia amezisisitizia halmashauri zilizopokea fedha hizo kuzitumia kwa malengo yaliyokusudiwa ambayo ni kukarabati miradi ya maji iliyopo vijijini, kuanzisha na kuimarisha jumuiya za watumia maji pamoja na kutunza na kuhifadhi vyanzo vya maji.




Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akizungumza na fundi anayejenga mnara wa kuweka tanki la maji la lita elfu 10 katika kijiji cha Ghalunyangu, Wilayani Singida.

Mhandisi wa Maji Mkoa wa Singida Mhandisi Lydia Joseph (aliyeinama) akikagua mabomba yatakayotumika kupeleka maji kwenye vituo vitatu vya kuchotea maji katika kijiji cha Ghalunyangu, Wilayani Singida.

Wanakijiji cha Ghalunyangu wakichota maji katika bomba pekee lililopo katika chanzo cha maji na maradi wa maji kijijini hapo. Fedha za malipo kwa matokeo zimeelekezwa kijijini hapo ili kujenga vituo vitatu vya kuchotea maji kwa kuanzia ikiwa vituo vingine vitajengwa hapo baadaye.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akizungumza na wana kijiji cha Ghalunyangu, Wilayani Singida waliokusanyika katika chanzo cha maji na eneo ulipo mradi wa maji kijjini hapo.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad

Responsive Ads Here